Ijumaa, 12 Julai 2013

WAIMBAJI WA INJILI AFRIKA YA KUSINI WAKUSANYIKA NJE YA HOSPITALI ALIYOLAZWA MANDELA

Solly na Deborah katikati wakiimba na wenzao nje ya hospitali kumtakia afya njema mzee Madiba.©statesman.com
Kundi la waimbaji muziki wa injili nchini Afrika ya kusini jumatano wiki hii walikusanyika nje ya hospitali ya Medi-clinic Heart alikolazwa baba wa taifa hilo mzee Nelson Mandela jijini Pretoria akipatiwa matibabu ya ugonjwa ambapo walikuwa wamebeba maua kumtakia afya njema.

Kundi hilo la wanamuziki wapatao 10 wakiongozwa na mchungaji Solly Mahlangu na mwanamama Debora Frazer na waimbaji wengineo walikaririwa wakisema kuwa, kama waimbaji muziki wa injili nchini humo walifika hospitalini hapo kuonyesha upendo wao na heshima kwa Rais huyo mstaafu ambaye wanasema bado wanamuhitaji, ambapo walitumia muda nje ya hospitali hiyo wakiimba pamoja  na kufanya maombi kwa kiongozi huyo mstaafu.

Aidha mwimbaji anayeitwa Zanele Mbokazi amesema wao hawana fedha wala dhahabu lakini wanalo jina la Yesu ambalo ndio wanalolitoa kwa mzee Madiba na familia yake.Kwa upande wake Deborah amelitaka taifa hilo kuendelea na maombi juu ya mzee Madiba kwakuwa nchi hiyo na dunia kwa ujumla bado wanamuhitaji mzee Madiba "Ni baba wa kwetu sote, Mungu ampe maisha marefu zaidi duniani", amesema Deborah



Ni siku ya 35 tangu mzee Madiba kupelekwa hospitalini hapo kwa matibabu kutokana na maradhi ya mapafu yanayomfanya kushindwa kupumua vyema. Huku mzozo ambao ulikuwa umeigubika familia yake kuhusiana na masuala ya maziko yameonekana kumalizwa kama wajukuu wa mzee huyo walivyonukuliwa na vyombo vya habari wakijibu maswali ya watu waliokuwa wakiwauliza maswali kwenye mtandao wa twitter.

Chanzo : IOL

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...