Katika hali ambayo inaashiria kwamba usalama wa watu na mali zao katika uwanja wa taifa hususan siku za matamasha hautoshi, mtangazaji na fundi mitambo wa WAPO Radio FM, Filemon Rupia, maarufu kama Father Filemon Rupia, amevamiwa usiku wa tamasha la matumaini na watu wasiojulikana, ambapo walimpora vitu kadhaa ikiwemo simu zake, pesa na kisha kumkata na kitu kinachosadikiwa kuwa ni kisu kwenye koo lake.
Tukio hilo linasemekeana kutokea majira ya saa mbili usiku, ambapo Filemon Rupia na wafanyakazi wenzake wakitokea kwenye ibada ya ujazo wa Roho Mtakatifu maeneo ya Mbezi Beach inayofahamika kama Oparesheni Takasika, walifika maeneo ya uwanja wa taifa, ambapo Father Rupia aliamua kurejea nyumbani kutokana na uchovu, ambapo wenzake walimuacha kwenye lango la kuingia uwanjani - ambapo alianza kutafuta usafiri wa kurudi nyumbani kwake.
Laiti kama angejua kilicho mbele yake, hakika angeingia na wenzake uwanjani, lakini mwanadamu ni mwanadamu tu. Kilichotokea wakati akitafuta usafiri ndio hiki tunachozungumza sasa, kuvamiwa, kuporwa, na kukatwa na kisu kwenye koo lake, ambapo haijajulikana lengo hasa la wavamizi hao kufanya hivyo ilikuwa ni nini.
Hata hivyo Mungu ashukuriwe, kwani kwa hivi sasa Filemon Rupia anaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma kwenye hospitali ya Kairuki, amapo alishonwa nyuzi kadhaa kwa ndani na nje ya koo. Tutakufikishia taarifa zaidi pindi ambapo tutazipokea kutoka kwenye vyanzo vyetu. Kwa hivi sasa anahitaji maombi yako kuvuka hali aliyonayo.
Maelezo ya Rupia
Hatimaye baada ya kufanya mawasiliano na Rupia, anaeleza kuwa akiwa anataka kuchukua bodaboda eneo la uwanja wa taifa, ndipo hapo dhahama lilitokea.
Bodaboda mbili zilikataa kwa maelezo kuwa kuna mtu anasubiriwa, bodaboda ya tatu ikadai kuwa haiwezi kwenda mbali. Ndipo hapo akalazimika kusogelea bodaboda za mbele zaidi ili apelekwe nyumbani, kilichofatia hao ni roba ya mbao, na kuvamiwa na vijana kadhaa ambapo katika purukushani, walitoa kisu na kuanza kumkata kooni, ambapo kisu kilikata ubao na kumchana eneo la kidevu na shingo. Na kama sio ubao kuwepo katikati, basi yangekuwa mengine kwa hivi sasa.
Mara baada ya ya hapo, ikafuata kuzirai kwa dakika kadhaa, na alipozinduka, ndio akasogea hadi getini kuomba msaada, ambapo walikwenda hadi kituo cha Polisi kabla ya kuelekea hospitali ya Temeke (ambapo huduma zilikuwa hafifu) na baadae kurudi nyumbani kwa ajili ya kwenda hospitali ya Kairuki.
Wakati haya yote yanatokea, alikuwa akizungumza na mfanyakazi mwenzake, Joyce Mathew, ambaye baada kufuatilia tukio lote kupitia simu kuanzia wanamkaba na hadi kuiba mali zake, aliwasiliana na wakubwa zake, ambapo msaada ulifanikiwa kupatikana kwa wepesi zaidi.
Pamoja na yote haya, hapa ndipo tunakumbushwa kuwa kila mara jua likizama na tukalala na kuamka salama, basi sifa na utukufu tukumbuke kumrejeshea Yesu Kristo anayetawala muda wote.
source:gospelkitaa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni